Serikali Yatoa Taarifa Rasmi Kuhusu Mwenendo wa Influenza, UVIKO-19, Dengue na Kipindupindu Nchini Tanzania

Serikali Yatoa Taarifa Rasmi Kuhusu Mwenendo wa Influenza, UVIKO-19, Dengue na Kipindupindu Nchini Tanzania

Serikali Yatoa Tahadhari Kuhusu Influenza, UVIKO-19, Dengue na Kipindupindu

Dodoma | 25 Februari 2026

Muhtasari wa Taarifa Rasmi

Wizara ya Afya nchini Tanzania imetoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa magonjwa ya mlipuko nchini, ikieleza kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa wa mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 katika kipindi hiki cha msimu. Aidha, Wizara imetoa tahadhari kuhusu Homa ya Dengue kufuatia mvua za masika zinazoendelea, pamoja na mrejesho kuhusu hali ya Kipindupindu nchini.

Ongezeko la Influenza na UVIKO-19

Kwa mujibu wa takwimu za ufuatiliaji, kila mwaka katika kipindi cha Novemba hadi Aprili kumekuwa na ongezeko la maambukizi ya mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 nchini na duniani. Magonjwa haya huenezwa kupitia majimaji ya njia ya hewa wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza, na pia kwa kugusa mazingira yaliyoathiriwa.

Dalili zake ni pamoja na homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, kuwashwa koo na uchovu.

Wizara imesisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari zifuatazo:

  • Kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya
  • Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono
  • Kuepuka misongamano isiyo ya lazima
  • Kuvaa barakoa unapokuwa na dalili au unapokuwa kwenye maeneo yenye msongamano
  • Kuwahi kituo cha afya kupata matibabu stahiki na kuepuka matumizi holela ya antibiotiki

Tahadhari ya Homa ya Dengue

Kutokana na mvua za masika zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini, Wizara imetoa tahadhari kuhusu Homa ya Dengue, ugonjwa unaoenezwa na mbu aina ya Aedes. 

Dalili zake ni homa kali, maumivu ya kichwa na viungo, maumivu ya macho na uchovu, na zinaweza kufanana na dalili za Malaria.

Jamii imetakiwa:

  • Kutokomeza mazalia ya mbu kwa kuondoa maji yaliyotuama na taka zinazoweza kuhifadhi maji
  • Kujikinga dhidi ya mbu kwa kuvaa nguo ndefu, kutumia dawa za kufukuza mbu na kuweka nyavu madirishani
  • Kuwahi kituo cha afya mara tu dalili zinapoonekana

Hali ya Kipindupindu Nchini

Serikali imeeleza kuwa katika kipindi cha takriban mwezi mmoja uliopita hakujapatikana mgonjwa mpya wa Kipindupindu nchini, licha ya mlipuko uliokuwa umeathiri mikoa mingi awali. Hata hivyo, tahadhari inaendelea kutokana na mvua zinazoendelea na uwepo wa maambukizi katika nchi jirani.

Wananchi wamehimizwa kuendelea:

  • Kuchemsha au kutibu maji ya kunywa kwa dawa maalumu (aquatab/waterguard) na kuyatunza vizuri wakati wa matumizi
  • Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutoka chooni, baada ya kumhudumia mtoto aliyejisaidia na kabla ya kumyonyesha mtoto
  • Kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira safi
  • Kujenga na kutumia vyoo bora na kuviweka katika hali ya usafi nyakati zote
  • Kutunza usafi wa mazingira na vyanzo vya maji

Taarifa hii imetolewa na Dkt. Grace E. Magembe, Mganga Mkuu wa Serikali.

Wito wa TNA CARE kwa Umma

TNA CARE inawahimiza wananchi kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za Serikali na kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya ili kulinda afya binafsi, familia na jamii kwa ujumla.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali soma tamko rasmi la Wizara ya Afya.

Author

TNA CARE

Healthcare professionals dedicated to providing expert health tips and medical insights for our community.

Message
Hello, chat with us now!